Language 

Updates  | Medjugorje[EN]  | Messages  | News & Articles[EN]  | Videos[EN]  | Pictures & Photos[EN] | Site Map  | About[EN]

www.medjugorje.ws » Text version » Our Lady of Medjugorje Messages » Our Lady of Medjugorje Messages

Our Lady of Medjugorje Messages

Wanangu wapendwa, Fanyeni kazi na shuhudieni kwa upendo Ufalme wa Mbinguni ili muweze kuwa hamjambo hapa duniani. Wanangu, Mungu atabariki mara mia zaidi juhudi yenu na mtakuwa mashahidi katikati ya watu, roho za wale wasioamini zitahisi neema ya wongofu na Mbingu itazipokea taabu zenu na sadaka zenu. Wanangu, shuhudieni kwa tasbihi mkononi ili muwe wangu na kateni shauri kuwa watakatifu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.

Wanangu wapendwa, Upendo wa Mwanangu ni mkubwa. Laiti mngeweza kujua ukuu wa upendo Wake, msingeacha kamwe kumwabudu na kumshukuru. Yeye ni sikuzote hai pamoja nanyi katika Ekaristi, maana Ekaristi ni moyo Wake, Ekaristi ni moyo wa imani. Yeye hakuwaacha kamwe: hata wakati ninyi mlipojaribu kwenda mbali Naye, Yeye hakuwaacha kamwe.

Kwa hiyo, moyo wangu wa kimama unafurahi wakati unapotazama jinsi mlivyojaa upendo mnapomrudia, wakati unapoona ya kuwa mnamrudia kwa njia ya upatanisho, upendo na matumaini. Moyo wangu wa kimama unajua ya kuwa ikiwa mngetembea katika njia ya imani, mngekuwa kama machipukizi, kama matumba na kwa njia ya sala na kufunga mngekuwa kama matunda, kama maua, mitume wa upendo wangu, mngekuwa waleta mwanga na mngeangaza kwa upendo na hekima pande zote karibu nanyi.

Wanangu, kama mama, ninawaomba: salini, fikirini na kutafakari. Yote yanayowatokea, mazuri, ya kuumiza na ya kufurahisha, hayo yote yawasababisha kukua kiroho, yawafanya kuwa Mwanangu akue ndani yenu. Wanangu mkabidhi kwake. Mumwamini na mtumainie upendo Wake. Na Yeye awaongoze. Na Ekaristi iwe mahali mtakapolisha roho zenu ili kueneza upendo na ukweli. Shuhudieni Mwanangu. Ninawashukuru.

Wanangu wapendwa, mwaliko wangu kwenu ni sala. Sala iwe kwenu furaha na taji la kuwaunganisha na Mungu. Wanangu, majaribu yatakuja nanyi hamtakuwa na nguvu na dhambi itatawala lakini mkiwa wangu, mtashinda maana kimbilio lenu litakuwa Moyo wa Mwanangu Yesu. Kwa hiyo wanangu, rudieni sala ili sala iwe maisha kwenu, mchana na usiku. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.

Wanangu wapendwa, kufuatana na matakwa ya Baba mwenye rehema, nimewapa na tena nitawapa ishara dhahiri za uwepo wangu wa kimama. Wanangu, ishara hizo ni kwa hamu yangu ya kimama ya kuziponya roho. Ishara hizo ni kwa hamu ya kuwa kila mwanangu awe na imani ya kweli, aishi mang’amuzi ya ajabu akinywa kwenye chemchemi ya Neno la Mwanangu, Neno la uhai. Wanangu, kwa njia ya upendo wake na sadaka, Mwanangu alichukua ulimwenguni mwanga wa imani na aliwaonyesheni njia ya imani. Maana, wanangu, imani huamsha huzuni na maumivu. Imani ya kweli hufanya sala kusisika zaidi, hutimiza matendo ya huruma: mazungumzo na matoleo. Wale wanangu walio na imani, imani ya kweli, ni wenye heri pamoja na yote, maana wanaishi duniani mwanzo wa heri ya Mbinguni. Kwa hiyo, wanangu, mitume wa upendo wangu, ninawaalika kutoa mfano wa imani ya kweli, kupeleka mwanga pale palipo giza, kumwishi Mwanangu. Wanangu, kama Mama ninawaambia: hamwezi kupitia njia ya imani na kumfuata Mwanangu pasipo wachungaji wenu. Salini ili wawe na nguvu na upendo kwa kuwaongoza. Sala zenu ziwe sikuzote pamoja nao. Nawashukuru!

Wanangu wapendwa, Namshukuru Mungu kwa kila mmoja wenu. Hasa, wanangu, asanteni kwa kuitikia wito wangu. Mimi ninawatayarisha kwa nyakati mpya ili muwe imara katika imani na kusali daima, ili Roho Mtakatifu atende kwa njia yenu na afanye upya uso wa nchi. Ninasali pamoja nanyi kwa amani, karama ya thamani kuliko zote, hata ingawa shetani hutaka vita na machukio. Ninyi, wanangu, muwe mikono yangu inayonyoshwa na tembeeni katika kujivunia pamoja na Mungu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.

Wanangu wapendwa, moyo safi na wazi tu utawawezesha ninyi kumjua kweli Mwanangu, na wale wote wasiojua upendo wake kuujua kwa njia yenu. Upendo tu utawawezesha kuelewa kuwa ni wenye nguvu kuliko kifo, maana upendo wa kweli umeshinda kifo na umefanya hata kifo hakipo tena. Wanangu, msamaha ni mtindo bora wa upendo. Ninyi, kama mitume wa upendo wangu, yawapasa kusali kwa kuwa wenye nguvu katika roho na kuweza kuelewa na kusamehe. Ninyi, mitume wa upendo wangu, kwa njia ya ufahamu na msamaha, mnatoa mfano wa upendo na rehema. Kuweza kuelewa na kusamehe ni karama inayotokana na maombi na yatupasa kuitunza. Mkisamehe ninyi mnaonyesha ya kuwa mnajua kupenda. Tazameni, wanangu, kama Baba wa mbinguni anavyowapenda kwa upendo mkubwa, kwa ufahamu, kwa uelewa, msamaha na haki. Kama anavyowatolea mimi, Mama wa mioyo yenu. Na tazama: mimi nipo katikati yenu ili kuwabariki kwa baraka ya kimama; ili kuwaalika kusali na kufunga; ili kuwasihi kuamini, kutumaini, kusamehe, kuwaombea wachungaji wenu na hasa kupenda bila mipaka. Wanangu, nifuateni! Njia yangu ni njia ya amani na upendo, njia ya Mwanangu. Ndiyo njia ya kuongoza katika ushindi wa Moyo wangu. Nawashukuru!

Wanangu wapendwa, Mungu kwa rehema yake alinijalia kuwa pamoja nanyi, ili kuwaelimisha na kuwaongoza kuelekea katika hatua ya wongofu. Wanangu, ninyi nyote mmeitwa kusali kwa moyo wenu wote ili mpango wa wokovu utimilike ndani mwenu na kwa njia yenu. Jueni wanangu, kwamba maisha ni mafupi na uzima wa milele unawangoja kwa kadiri ya mastahili yenu. Kwa hiyo salini, salini, salini ili muweze kuwa vyombo vya kufaa mikononi mwa Mungu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.

Wanangu wapendwa, kwa upendo wa kimama ninawaalika ili kwa moyo safi na wazi, kwa imani kabisa, mpokee upendo mkubwa wa Mwanangu. Mimi ninajua ukuu wa upendo wake, mimi nilimchukua ndani yangu, Hostia moyoni, Mwanga na Upendo wa ulimwengu. Wanangu, hata kuelekea kwangu kwenu ninyi ni ishara ya upendo na ya huruma ya Baba wa Mbinguni, ni tabasamu kilichojaa upendo wa Mwanangu, ni mwaliko kwa uzima wa milele. Damu ya Mwanangu ilimwagika kwa ajili yenu kwa upendo. Ile Damu yenye thamani ni kwa wokovu wenu, kwa ajili ya uzima wa milele. Baba wa mbinguni aliumba mtu kwa ajili ya furaha ya milele. Haiwezekani ninyi kufa, ninyi mnaojua upendo wa Mwanangu, ninyi mnaomfuata. Uzima umeshinda: Mwanangu yu hai! Kwa hiyo, wanangu, mitume wa upendo wangu, sala iwaonyeshe njia, jinsi ya kueneza upendo wa Mwanangu kwa jinsi ilivyo bora zaidi. Wanangu, hata wakati mnapojaribu kuishi maneno ya Mwanangu, ninyi mnasali. Wakati mnapowapenda watu mnaokutana nao, mnaeneza upendo wa Mwanangu. Upendo ni neno linalofungua milango ya Uzima. Wanangu, tangu awali nimesali kwa ajili ya Kanisa. Kwa hiyo ninawaalika nanyi, mitume wa upendo wangu, kusali kwa ajili ya Kanisa na watumishi wake, kwa wale ambao Mwanangu amewaita. Nawashukuru.

Wanangu wapendwa! Wakati huu ndio wakati wa neema, wakati wa rehema kwa kila mmoja wenu. Wanangu, msiruhusu upepo wa chukio na hofu utawale ndani yenu na karibu nanyi. Ninyi, wanangu, mmealikwa kuwa upendo na sala. Ibilisi ataka hofu na fujo lakini ninyi, wanangu, muwe furaha ya Yesu Mfufuka ambaye amekufa na kufufuka kwa ajili ya kila mmoja wenu. Yeye ameshinda kifo kwa kuwapeni uzima, uzima wa milele. Kwa hiyo, wanangu, mshuhudieni na muwe wenye fahari kwa kufufuliwa katika Yeye. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.

Wanangu wapendwa, kama Mama ambaye anajua wana wake, ninajua ya kuwa mnamtamani Mwanangu. Ninajua ya kuwa mnatamani ukweli, amani, na kilicho chema wala si uovu. Kwa sababu hiyo mimi, kama Mama, kwa njia ya upendo wa Mungu ninawaita ninyi na kuwaalika ili, mkisali kwa moyo safi na wazi, mmtambue ninyi wenyewe Mwanangu, upendo wake, na Moyo wake wenye rehema. Mwanangu alikuwa akiona uzuri katika vitu vyote. Yeye anatafuta mema, hata yale mema madogo yanayofichika, katika roho zote, ili kusamehe maovu. Kwa hiyo, wanangu, mitume wa upendo wangu, ninawaalika kumwabudu, kumshukuru daima na kumstahili. Maana yeye aliwaambieni maneno ya kimungu, maneno ya Mungu, maneno yaliyo kwa watu wote na hata milele. Kwa hiyo, wanangu, ishini uchangamfu, umakini, umoja na muwe na mapenzi baina yenu. Haya mnapaswa kuwa nayo katika ulimwengu wa leo: hivyo mtakuwa mitume wa upendo wangu, hivyo mtashuhudia Mwanangu kwa jinsi ya haki. Nawashukuru.

To compare Medjugorje messages with another language versions choose
<<Previous  1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 ... 23 Next>>

 

PC version: This page | Medjugorje | Apparitions[EN]  | Our Lady of Medjugorje Messages  | Medjugorje News & Articles[EN]  | Pictures & Photos[EN]  | Medjugorje Videos[EN]