Language 

Updates  | Medjugorje[EN]  | Messages  | News & Articles[EN]  | Videos[EN]  | Pictures & Photos[EN] | Site Map  | About[EN]

www.medjugorje.ws » Text version » Our Lady of Medjugorje Messages » Our Lady of Medjugorje Messages

Our Lady of Medjugorje Messages

Wanangu wapendwa, ninawaalika kupokea kwa unyofu wa moyo maneno yangu, ninayowaambieni kama Mama ili muende katika njia ya mwanga kamili, wa usafi, wa upendo wa pekee wa Mwanangu, mtu na Mungu. Raha, mwanga usioelezeka kwa maneno ya kibinadamu utaingia nafsini mwenu, na mtashikwa na amani na upendo wa Mwanangu. Ninataka hayo kwa wanangu wote. Kwa hiyo ninyi, mitume wa upendo wangu, ninyi mnaojua kupenda na kusamehe, ninyi msiohukumu, ninyi ambao mimi ninahimiza, muwe mfano kwa wale wote wasiokwenda katika njia ya mwanga na upendo au waliotengana nayo. Kwa njia ya maisha yenu waonyesheni ukweli, waonyesheni upendo, maana upendo hushinda matatizo yote, na wanangu wote wana kiu ya upendo. Ushirika wenu wa upendo ni zawadi kwa Mwanangu na kwangu. Lakini, wanangu, kumbukeni ya kuwa kupenda maana yake ni kupenda mwenzako na kutakia wongofu wa nafsi yake. Ninapowatazama mmekusanyika karibu nami, moyo wangu unahuzunika kwa sababu ninaona upendo haba wa kidugu, upendo wenye huruma. Wanangu, Ekaristi, Mwanangu hai katikati yenu, na maneno yake yatawasaidia kuelewa. Neno lake, kweli, ni uhai, Neno lake huburudisha nafsi, Neno lake huwajulisha upendo. Wanangu wapenzi, ninawaombeni tena, kama Mama apendaye wana wake: wapendeni wachungaji wenu, waombeeni… Nawashukuru!

Wanangu wapendwa, katika wakati huo wa wasiwasi ninawaalika kumwamini zaidi Mungu aliye Baba yenu mbinguni na anayenituma kuwaongozeni kwake. Ninyi, mfungulieni mioyo yenu kwa zawadi ambazo Yeye ataka kuwapeni na katika kimya ya moyo wenu mwabuduni Mwanangu, aliyetolea maisha Yake ili muishi katika milele anakotaka kuwaongoza. Matumaini yenu na yawe furaha ya kukutana na Yule Aliye juu katika maisha ya kila siku. Kwa hiyo ninawaalika: msiache sala maana sala hutenda miujiza. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.

Wanangu wapendwa, Mwanangu, aliye mwanga wa upendo, yote aliyoyafanya na anayoyafanya hufanya kwa ajili ya upendo. Vivyo hivyo nanyi, wanangu, mnapoishi katika upendo, mnapompenda jirani yenu na mnapofanya mapenzi yake. Enyi mitume wa upendo wangu, jifanyeni wadogo! Mfungulieni Mwanangu mioyo yenu safi, ili Yeye aweze kutenda kazi kwa njia yenu. Kwa msaada wa imani, mjijazie upendo. Lakini, wanangu, msisahau ya kuwa Ekaristi ndiyo kiini cha imani. Yeye ndiye Mwanangu anayewalisheni kwa Mwili wake na kuwaimarisheni kwa Damu yake. Yeye ndiye ajabu ya upendo: Mwanangu ajaye tena mwenye uhai ili kuzifufua nafsi. Wanangu, mkiishi katika upendo, ninyi mnafanya mapenzi ya Mwanangu naye huishi ndani yenu. Wanangu, matakwa yangu ya kimama ni kwamba mpendeni zaidi na zaidi, maana Yeye anawapenda kwa upendo wake. Anawapa upendo wake ili muweze kuueneza kwa watu wote kandokando yenu. Kwa njia ya upendo wake, kama mama mimi nipo pamoja nanyi kuwaambieni maneno ya upendo na matumaini, kuwaambieni maneno ya milele na ya kushinda wakati na mauti, kuwaalikeni kuwa mitume wangu wa upendo. Nawashukuru!

Wanangu wapendwa, leo pia ninawaalika kuishi pamoja na Yesu maisha yenu mapya. Bwana Mfufuka awape nguvu ili muwe daima mashujaa katika majaribu ya maisha, na waaminifu na mdumu katika kusali, maana Yesu aliwaokoeni kwa majeraha Yake na kwa njia ya Ufufuko Wake aliwapa maisha mapya. Salini, wanangu na msipoteze matumaini. Katika mioyo yenu na ziwe furaha na amani, muwe mashahidi ya furaha ya kuwa wangu. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwapenda nyote kwa upendo wangu wa kimama. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.

Wanangu wapendwa, kwa njia ya upendo mkubwa wa Baba wa Mbinguni, mimi ni pamoja nanyi kama Mama yenu nanyi ni pamoja nami kama wanangu, kama mitume wa upendo wangu ambao ninakusanya daima karibu nami. Wanangu, ninyi ni wale ambao, mkisali, yawapasa kujitolea kabisa kwa Mwanangu, ili kwamba si ninyi tena mnaoishi, bali ni Mwanangu ndani yenu; ili wale wote wasiomjua wamwone ndani yenu na watake kumjua. Salini ili waone ndani yenu unyenyekevu thabiti na wema, utayari kuwatumikia wengine; waone kwamba mnaishi kwa moyo wito wenu duniani, mkishirikiana na Mwanangu. Waone ndani yenu upole, rehema na upendo kuelekea Mwanangu, kama vile kuelekea ndugu na dada zenu. Enyi mitume wa upendo wangu, hamna budi kusali sana na kutakasa mioyo yenu, ili ninyi muwe wale wa kwanza waendao katika njia ya Mwanangu; ili ninyi muwe wale wenye haki wanaoungana na haki ya Mwanangu. Wanangu, kama mitume wangu lazima muungane na ushirika utokao katika Mwanangu, ili wanangu wasiomjua Mwanangu watambue ushirika wa upendo na watake kutembea katika njia ya uzima, njia ya umoja na Mwanangu. Nawashukuru.

Wanangu wapendwa, ninawaalika kukaa pamoja nami katika kusali, wakati huu wa neema, ambapo giza linapigana na mwagaza. Wanangu, salini, muungame dhambi zenu mkaanzishe maisha mapya katika neema. Kateni shauri kwa Mungu naye atawaongoza kuelekea utakatifu na msalaba utakuwa kwenu ishara ya ushindi na matumaini. Mjivunie kubatizwa na mshukuruni moyoni mwenu kushika mpango wa Mungu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.

Wanangu wapendwa, Baba wa Mbinguni amenifanyia makuu, jinsi anavyowafanyia wale wote wanaompenda sana na kwa wema na uaminifu na wanaomtumikia kwa ibada. Wanangu, Baba wa Mbinguni anawapenda na kwa ajili ya upendo wake mimi nipo hapa pamoja nanyi. Ninasema nanyi: kwa nini hamtaki kuona ishara? Pamoja naye yote ni rahisi zaidi: hata mateso, tunayoishi pamoja naye, ni mepesi zaidi, maana kuna imani. Imani husaidia mateso, na maumivu pasipo imani huongoza katika kukata tamaa. Mateso tunayoyaishi na kuyatolea kwa Mungu, huinua mtu. Je, Mwanangu hakuukomboa ulimwengu kwa njia ya mateso yake makali? Mimi, kama mama yake, katika maumivu na mateso nilikaa pamoja naye, kama vile ninavyokaa pamoja nanyi. Wanangu, mimi nipo pamoja nanyi katika maisha: katika maumivu na mateso, katika furaha na upendo. Kwa hiyo muwe na matumaini: matumaini ndiyo yanayotuwezesha kuelewa ya kuwa hapa, kwenye mateso, ni uhai. Wanangu, mimi nasema nanyi; sauti yangu inasema na nafsi yenu, Moyo wangu unasema na moyo wenu: Enyi, mitume wa upendo wangu, Moyo wangu wa kimama jinsi gani unavyowapenda. Mambo haya nataka kuwafundisha. Jinsi gani Moyo wangu unataka muwe wakamilifu, lakini mtakuwa hivyo tu wakati nafsi, mwili na upendo yatakapoungana ndani yenu. Kama wanangu nawaombeni: salini sana kwa ajili ya Kanisa na kwa wahudumu wake, kwa wachungaji wenu, ili Kanisa liwe kama Mwanangu anavyolitaka: safi kama maji ya chemchemi na limejaa upendo. Nawashukuru.

Wanangu wapendwa! Katika kipindi hiki cha neema ninawaalika nyote kujifungua na kuishi amri ambazo Mungu aliwapeni ili, kwa njia ya sakramenti, ziwaongoze katika njia ya wongofu. Ulimwengu na vishawishi vya ulimwengu vinawajaribu; ninyi, wanangu, angalieni viumbe vya Mungu ambavyo katika uzuri na unyenyekevu Yeye aliwapa, na mpendeni Mungu, enyi wanangu, kuliko kila kitu naye atawaongoza katika njia ya wokovu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.

Wanangu wapendwa, ninyi ambao Mwanangu anawapenda, ninyi ambao mimi ninawapenda, msiruhusu ubinafsi, kujipenda wenyewe, zitawale duniani. Msiache upendo na wema zifichwe. Ninyi mnaopendwa, mliojua upendo wa Mwanangu, kumbukeni ya kuwa kupendwa maana yake ni kupenda. Wanangu, muwe na imani! Mnapokuwa na imani mnafurahi na mkaeneza amani, nafsi yenu inaruka kwa shangwe: katika nafsi ile yumo Mwanangu. Mnapojitolea wenyewe kwa ajili ya imani, mnapojitolea wenyewe kwa ajili ya upendo, mnapowafanyia watu wengine mema, Mwanangu hutabasamu katika nafsi yenu. Mitume wa upendo wangu, mimi, kama Mama, ninawaelekea, ninawakusanya kunizunguka na ninataka kuwaongozeni katika njia ya upendo na imani, katika njia ya kufika kwenye Nuru ya ulimwengu. Nipo hapa kwa upendo na kwa imani, kwa maana, kwa baraka yangu ya kimama, nataka kuwapeni matumaini na nguvu katika mwendo wenu, kwa sababu njia ya kuongoza kwa Mwanangu si rahisi: imejaa matendo ya kujinyima, ya kujitolea, ya kujidhabihu, ya kusamehe na ya upendo, upendo mwingi. Njia ile, lakini, hupata amani na furaha. Wanangu, msisadiki sauti za uongo zinazosemesha kwa maneno yasiyo na ukweli, mwanga usio wa ukweli. Ninyi wanangu rudini kwa Maandiko! Ninawaangalieni kwa upendo kupita kiasi na, kwa neema ya Mungu, ninajidhihirisha kwenu. Wanangu, njoni pamoja nami, nafsi yenu iruke kwa shangwe! Nawashukuru.

Wanangu wapendwa! Kipindi hiki kiwe kwenu kipindi cha sala ili Roho Mtakatifu, kwa njia ya sala, ashuke juu yenu na awape wongofu. Fungueni mioyo yenu na someni Maandiko Matakatifu ili, kwa njia ya ushahidi, ninyi pia muweze kuwa karibu zaidi na Mungu. Wanangu, tafuteni hasa Mungu na vitu vya Mungu na acheni duniani vile vya dunia, maana Shetani huwavuta kwa mavumbi na dhambi. Ninyi mnaalikwa katika njia ya utakatifu na mmeumbwa kwa ajili ya Mbingu. Tafuteni, kwa hiyo, Mbingu na vitu vya mbinguni. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.

To compare Medjugorje messages with another language versions choose
<<Previous  1 ... 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21 ... 23 Next>>

 

PC version: This page | Medjugorje | Apparitions[EN]  | Our Lady of Medjugorje Messages  | Medjugorje News & Articles[EN]  | Pictures & Photos[EN]  | Medjugorje Videos[EN]