Language 

Updates  | Medjugorje[EN]  | Messages  | News & Articles[EN]  | Videos[EN]  | Pictures & Photos[EN] | Site Map  | About[EN]

www.medjugorje.ws » Text version » Our Lady of Medjugorje Messages » Our Lady of Medjugorje Messages containing 'nawaombeni'

Our Lady of Medjugorje Messages containing 'nawaombeni'

Total found: 6
Wanangu wapendwa! Mimi Mama yenu, ninyi mliokusanyika hapa na Mama wa ulimwengu mzima, nawabariki kwa baraka ya kimama na kuwaalika kuanza safari katika njia ya unyenyekevu. Njia hiyo inawaongoza katika ujuzi wa upendo wa Mwanangu. Mwanangu ni Mwenye uwezo. Yeye yumo katika kila kitu. Kama ninyi, wanangu, hamelewi hayo, basi mtambue kuwa katika roho yenu giza na upofu zinatawala. Unyenyekevu tu huweza kuwaponya. Wanangu, mimi nilikuwa nimeishi daima kwa unyenyekevu, kwa uhodari na kwa matumaini. Nilijua, nilikuwa nimeelewa ya kuwa Mungu yu ndani yetu na sisi ndani ya Mungu. Nawaombeni kuelewa vile vile. Nataka ninyi nyote muwe pamoja nami katika umilele, maana ninyi ni sehemu yangu. Katika njia yenu nitawasaidia. Upendo wangu utawafunika kama joho na kuwafanya ninyi mitume wa mwanga wangu, wa mwanga wa Mungu. Kwa upendo utokao katika unyenyekevu, mtaleta mwanga palipotawala giza na upofu. Mtaleta Mwanangu, aliye mwanga wa ulimwengu. Mimi ni sikuzote kando ya wachungaji wenu na kusali ili wawe siku zote kwenu mfano wa unyenyekevu. Nawashukuru!

Wanangu wapendwa, kwa upendo wa kimama nawaombeni: pendaneni! mioyoni mwenu muwe kama Mwanangu alitaka tangu awali: kwanza kabisa kumpenda Baba wa Mbinguni na kuwa na upendo kwa jirani yenu, kuliko yote yaliyopo hapa duniani. Wanangu wapendwa, hamtambui dalili za nyakati hizi? Hamtambui ya kuwa yote yanayotokea kando kando yenu, hutokea kwa sababu hakuna upendo? Fahamuni kwamba wokovu hupatikana katika thamani za kweli, pokeeni uweza wa Baba wa Mbinguni, mpendeni na kumheshimu. Fuateni njia ya Mwanangu. Ninyi, wanangu, mitume wangu wapenzi, mnakusanyika siku zote daima kunizunguka maana mna kiu, mna kiu ya amani, ya upendo na ya furaha. Kateni kiu yenu katika mikono yangu! Mikono yangu yawatolea Mwanangu, aliye chemchemi ya maji safi. Yeye atafufua imani yenu na kusafisha mioyo yenu, kwa sababu Mwanangu hupenda kwa moyo safi na mioyo iliyo safi humpenda Mwanangu. Mioyo safi tu ndiyo minyenyekevu na yenye imani thabiti. Wanangu, nawaombeni ya kuwa na mioyo ya namna hii! Mwanangu aliniambia ya kuwa Mimi ni Mama wa ulimwengu wote: nawaombeni ninyi, mnaonipokea kama Mama, ili kwa maisha yenu, sala na sadaka nisaidieni ili wanangu wote wanipokee kama Mama, niweze kuwaongoza kwenye chemchemi ya maji safi. Nawashukuru! Wanangu wapenzi, wachungaji wenu wanapowatolea mwili wa Mwanangu, mshukuruni Mwanangu daima moyoni mwenu kwa sadaka yake na kwa wachungaji anayewajalia siku zote.

Wanangu wapendwa, nipo hapa katikati yenu. Ninawatazama, ninawapa tabasamu na kuwapenda kama mama peke yake awezavyo kufanya. Kwa neema ya Roho Mtakatifu ajaye kwa njia ya usafi wangu, ninaona mioyo yenu na kuitolea kwa Mwanangu. Tangu muda mrefu nawaombeni muwe mitume wangu, na kusali kwa ajili ya wale wasioujua upendo wa Mungu. Naomba sala inayotokana na upendo, sala itoayo matunda na sadaka. Msipotee muda kutaka kuelewa kama mnastahili kuwa mitume wangu, Baba aliye Mbinguni atahukumu wote, lakini ninyi mpendeni na msikilizeni. Najua ya kuwa mambo hayo yote yanawafadhaisha, hata ujio wangu katikati yenu, lakini upokeeni kwa furaha na salini ili muelewe kwamba mnastahili kufanya kazi kwa ajili ya ufalme wa mbingu. Upendo wangu ni juu yenu. Salini ili upendo wangu udumu ndani ya kila moyo, kwa maana upendo huo unaosamehe ujitolea bila kukata tamaa. Nawashukuru.

Wanangu wapendwa, nawaalika kueneza imani katika Mwanangu, imani yenu. Ninyi wanangu, mlioangazwa na Roho Mtakatifu, mitume wangu, itangazeni imani kwa watu wengine, yaani kwa wasiosadiki, wasioijua na wasiotaka kuijua. Kwa sababu hiyo yawapasa kusali sana kwa ajili ya zawadi ya upendo, maana upendo ndio alama maalum ya imani ya kweli, na ninyi mtakuwa mitume wa upendo wangu. Upendo hufanya upya daima maumivu na furaha ya Ekaristi, hufanya upya maumivu ya Mateso ya Mwanangu, aliyewaonyesha upendo usio na kifani; hufanya upya furaha ya tendo la kuwaachia Mwili wake na Damu yake kwa ajili ya kuwalisha na hivyo kuwa kitu kimoja nanyi. Nikiwaangalia kwa wema nahisi upendo pasipo kiasi, ulioniimarisha katika hamu yangu ya kuwaongoza katika imani thabiti. Imani thabiti itawapa furaha na uchangamfu duniani, na mwishowe kuwaunganisha na Mwanangu. Hiyo ndiyo hamu yake. Kwa hiyo mwishi katika Yeye, na katika upendo, isheni katika nuru iliyowaangaza daima katika Ekaristi. Nawaombeni kusali sana kwa wachungaji wenu, kusali ili kupata upendo mkubwa kwa ajili yao, kwa maana Mwanangu aliwapeni ili waweze kuwalisha kwa Mwili wake na kuwafundisha upendo. Kwa hiyo wapendeni ninyi pia! Lakini, wanangu, kumbukeni: upendo maana yake ni kuvumilia na kutoa na kutohukumu kamwe. Nawashukuru.

Wanangu wapendwa, nataka kuongea nanyi tena juu ya upendo. Nimewakusanya kunizunguka kwa Jina la Mwanangu, kwa kadiri ya mapenzi yake. Nataka imani yenu iwe thabiti na iwe inatokana na mapendo, kwa maana wanangu wale wanaoelewa upendo wa Mwanangu na kuufuata, huishi katika mapendo na matumaini. Wamejua upendo wa Mungu. Kwa hiyo, wanangu, salini, salini ili muweze kupenda zaidi muwezavyo na kutenda matendo ya upendo. Kwa maana, imani peke yake, pasipo upendo wala matendo ya upendo, si neno ninaloomba kwenu. Wanangu, ule ni utovu wa imani, ni kujisifu mwenyewe. Mwanangu hutaka imani na matendo, upendo na wema. Mimi ninasali, lakini nawaombeni pia kusali na kuishi upendo, kwa maana nataka ya kuwa Mwanangu, atakapoona mioyo ya wanangu wote, aweze kuona ndani yake upendo na wema, sio chukio na ubaridi. Wanangu, mitume ya upendo wangu, msipoteze tumaini, msikate tamaa: ninyi mnaweza kufanya! Mimi ninawapeni moyo na kuwabariki, maana yote yaliyopo duniani hapa - ambayo kwa bahati mbaya wanangu wengi huweka mahali pa kwanza - yatatoweka na upendo na matendo ya upendo tu zitabaki, nazo zitawafungulia malango ya Ufalme wa Mbinguni. Nitawangojea karibu na malango hayo, karibu na malango hayo nataka kuwangojea na kuwakumbatia wanangu wote. Nawashukuru.

Wanangu wapendwa, Baba wa Mbinguni amenifanyia makuu, jinsi anavyowafanyia wale wote wanaompenda sana na kwa wema na uaminifu na wanaomtumikia kwa ibada. Wanangu, Baba wa Mbinguni anawapenda na kwa ajili ya upendo wake mimi nipo hapa pamoja nanyi. Ninasema nanyi: kwa nini hamtaki kuona ishara? Pamoja naye yote ni rahisi zaidi: hata mateso, tunayoishi pamoja naye, ni mepesi zaidi, maana kuna imani. Imani husaidia mateso, na maumivu pasipo imani huongoza katika kukata tamaa. Mateso tunayoyaishi na kuyatolea kwa Mungu, huinua mtu. Je, Mwanangu hakuukomboa ulimwengu kwa njia ya mateso yake makali? Mimi, kama mama yake, katika maumivu na mateso nilikaa pamoja naye, kama vile ninavyokaa pamoja nanyi. Wanangu, mimi nipo pamoja nanyi katika maisha: katika maumivu na mateso, katika furaha na upendo. Kwa hiyo muwe na matumaini: matumaini ndiyo yanayotuwezesha kuelewa ya kuwa hapa, kwenye mateso, ni uhai. Wanangu, mimi nasema nanyi; sauti yangu inasema na nafsi yenu, Moyo wangu unasema na moyo wenu: Enyi, mitume wa upendo wangu, Moyo wangu wa kimama jinsi gani unavyowapenda. Mambo haya nataka kuwafundisha. Jinsi gani Moyo wangu unataka muwe wakamilifu, lakini mtakuwa hivyo tu wakati nafsi, mwili na upendo yatakapoungana ndani yenu. Kama wanangu nawaombeni: salini sana kwa ajili ya Kanisa na kwa wahudumu wake, kwa wachungaji wenu, ili Kanisa liwe kama Mwanangu anavyolitaka: safi kama maji ya chemchemi na limejaa upendo. Nawashukuru.

To compare Medjugorje messages with another language versions choose

 

PC version: This page | Medjugorje | Apparitions[EN]  | Our Lady of Medjugorje Messages  | Medjugorje News & Articles[EN]  | Pictures & Photos[EN]  | Medjugorje Videos[EN]