Language 

Updates  | Medjugorje[EN]  | Messages  | News & Articles[EN]  | Videos[EN]  | Pictures & Photos[EN] | Site Map  | About[EN]

www.medjugorje.ws » Text version » Our Lady of Medjugorje Messages » Our Lady of Medjugorje Messages

Our Lady of Medjugorje Messages

Wanangu wapendwa, Leo pia nawaletea Mwanangu Yesu katika mikono yangu, na kwa mikono hiyo nawapeni amani Yake na hamu ya Mbinguni. Ninasali pamoja nanyi kwa ajili ya amani na ninawaalika muwe amani. Nawabariki wote kwa baraka yangu ya kimama na ya amani. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.

Wanangu wapendwa, miaka hii yote ambapo Mungu ananijalia kuwepo pamoja nanyi ni ishara ya upendo mwingi sana wa Mungu kwa kila mmoja wenu na ishara ya jinsi alivyowapenda. Wanangu, Yeye Aliye Juu amewapeni neema nyingi na anataka kuwapa neema nyingi zaidi. Lakini, wanangu, mioyo yenu imefungwa, inaishi katika hofu na hayaruhusu upendo wa Yesu na amani yake yapate nafasi katika mioyo yenu na kutawala maisha yenu. Kuishi pasipo Mungu ni kuishi gizani wala kutoujua kamwe upendo wa Baba na ulinzi wake kwa kila mmoja wenu. Kwa hiyo wanangu, leo hasa mwombeni Yesu ili tangu leo maisha yenu yapate kuzaliwa upya katika Mungu, na maisha yenu iwe nuru itokayo kwenu. Namna hii mtakuwa mashahidi wa uwepo wa Mungu ulimwenguni hasa kwa kila mtu aishiye gizani. Wanangu, nawapenda na kuwaombeeni kila siku kwake Yeye Aliye Juu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.

Wanangu wapendwa, mimi ni sikuzote pamoja nanyi, kwa maana Mwanangu alinikabidhi ninyi. Nanyi, wanangu, mnanihitaji mimi, mnitafute, mnijie na mfurahishe Moyo wangu wa kimama. Mimi ninawapenda na nitawapenda ninyi mnaoteseka na kutolea mateso yenu kwa ajili ya Mwanangu na kwa ajili yangu. Upendo wangu hutafuta upendo wa wanangu wote na wanangu wote hutafuta upendo wangu. Kwa njia ya upendo Yesu hutafuta ushirika kati ya Mbingu na dunia, kati ya Baba wa mbinguni na ninyi, wanangu, Kanisa lake. Kwa hiyo lazima kusali sana, kusali na kulipenda Kanisa ambalo ninyi ni wake. Sasa Kanisa linateseka na kuhitaji mitume ambao, wakipenda ushirika, wanaposhuhudia na kutoa, waonyeshe njia za Mungu. Kanisa linahitaji mitume ambao, wakiishi Ekaristi kwa moyo, watende matendo makuu. Kanisa linawahitaji ninyi, mitume wangu wa upendo. Wanangu, Kanisa limeteswa na kusalitiwa tangu siku zake za awali, lakini linazidi kukua siku hata siku. Kanisa halitaharibiki, kwa maana Mwanangu alilipa moyo: Ekaristi. Nuru ya ufufuo wake imeng’aa na itang’aa juu yake. Kwa hiyo msiogope! Waombeeni wachungaji wenu, ili wawe na nguvu na upendo kwa kuwa madaraja ya wokovu. Nawashukuru.

Wanangu wapendwa, leo ninawaalika nyote: salini kwa ajili ya nia zangu. Amani ipo hatarini kwa hiyo wanangu, salini na muwe waletaji wa amani na matumani katika ulimwengu huu wa wasiwasi ambamo shetani anashambulia na kuleta majaribu ya kila aina. Wanangu muwe thabiti katika sala na imara katika imani. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwaombea ninyi nyote mbele ya Mwanangu, Yesu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.

Wanangu wapendwa, nataka kuongea nanyi tena juu ya upendo. Nimewakusanya kunizunguka kwa Jina la Mwanangu, kwa kadiri ya mapenzi yake. Nataka imani yenu iwe thabiti na iwe inatokana na mapendo, kwa maana wanangu wale wanaoelewa upendo wa Mwanangu na kuufuata, huishi katika mapendo na matumaini. Wamejua upendo wa Mungu. Kwa hiyo, wanangu, salini, salini ili muweze kupenda zaidi muwezavyo na kutenda matendo ya upendo. Kwa maana, imani peke yake, pasipo upendo wala matendo ya upendo, si neno ninaloomba kwenu. Wanangu, ule ni utovu wa imani, ni kujisifu mwenyewe. Mwanangu hutaka imani na matendo, upendo na wema. Mimi ninasali, lakini nawaombeni pia kusali na kuishi upendo, kwa maana nataka ya kuwa Mwanangu, atakapoona mioyo ya wanangu wote, aweze kuona ndani yake upendo na wema, sio chukio na ubaridi. Wanangu, mitume ya upendo wangu, msipoteze tumaini, msikate tamaa: ninyi mnaweza kufanya! Mimi ninawapeni moyo na kuwabariki, maana yote yaliyopo duniani hapa - ambayo kwa bahati mbaya wanangu wengi huweka mahali pa kwanza - yatatoweka na upendo na matendo ya upendo tu zitabaki, nazo zitawafungulia malango ya Ufalme wa Mbinguni. Nitawangojea karibu na malango hayo, karibu na malango hayo nataka kuwangojea na kuwakumbatia wanangu wote. Nawashukuru.

Wanangu wapendwa, sala yangu hata leo ni kwa ajili yenu nyote, hasa kwa wale walio na mioyo migumu kuitikia wito wangu. Mnaishi katika siku za neema wala hamtambui fadhili ambazo Mungu anawapeni kwa njia ya uwepo wangu. Wanangu, amueni hata leo kuwa watakatifu na jifunzeni kutokana na mifano ya watakatifu wa siku hizi na mtatambua ya kuwa utakatifu ni ukweli uliopo kwa ajili yenu nyote. Wanangu, furahini katika upendo kwa maana machoni pa Mungu ninyi ni wa pekee na hakuna atakayechukua nafasi ya mwingine, kwa maana ninyi ni furaha ya Mungu duniani hapa. Mshuhudieni amani, sala na upendo. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.

Wanangu wapendwa, nipo hapa katikati yenu kuwatieni moyo, kuwajaza kwa upendo wangu, kuwaalika tena kuwa mashahidi wa upendo wa Mwanangu. Wanangu wengi hawana tumaini, hawana amani, hawana upendo. Wao wanatafuta Mwanangu lakini hawajui jinsi wala wapi ya kumpata. Mwanangu awafungulia mikono Yake, nanyi wasaidieni ili waje mikononi Mwake. Wanangu, kwa hiyo ni lazima msali kwa upendo, lazima msali sana, sana, ili kupata upendo zaidi na zaidi, kwa maana upendo hushinda mauti na hudumisha maisha. Watume wa upendo wangu, wanangu wenye moyo mnyofu na safi, jiungeni zaidi na zaidi katika kusali. Mnatengana sana! Jipeni moyo katika kukua kiroho, kama vile Mimi ninawapeni moyo. Ninawaangalia na nipo karibu nanyi kila mnaponifikiria. Waombeeni wachungaji wenu, wale walioacha yote kwa ajili ya Mwanangu. Wapendeni na waombeeni, Baba wa Mbinguni husikiliza sala zenu. Nawashukuru.

Wanangu wapendwa, hata leo ninamwomba Roho Mtakatifu ili ajaze mioyo yenu kwa imani thabiti. Sala na imani zitajaza mioyo yenu kwa upendo na furaha, nanyi mtakuwa ishara kwa wale walio mbali na Mungu. Wanangu, mpeane moyo wenyewe kwa wenyewe ili kufanya sala ya moyo, ili sala iweze kujaza maisha yenu na ninyi, wanangu, kila siku muwe mashahidi wa utumishi: kwa Mungu katika kuabudu na kwa majirani zenu katika mahitaji yao. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwaombea ninyi nyote. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.

Wanangu wapendwa, wapendwa mitume wangu wa upendo, waletaji wangu wa ukweli, ninawaalika tena na ninawakusanya karibu nami ili mnisaidie, ili muwasaidie wanangu wote wenye kiu ya upendo na ukweli, wenye kiu ya Mwanangu. Mimi ndimi neema ya Baba wa Mbinguni iliyotumwa kuwasaidieni kuishi neno la Mwanangu. Pendaneni. Nimeyaishi maisha yenu duniani. Najua kwamba si kitu rahisi kila mara lakini, mkipendana, mtasali kwa moyo, mtafikia vilele vya maisha ya roho, na njia ya kwenda mbinguni itafunguliwa mbele yenu. Pale nawangojea mimi, Mama yenu, kwa maana mimi nipo pale. Muwe waaminifu kwa Mwanangu na muwafundishe wengine uaminifu. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwasaidia. Nitawafundisha imani, ili muweze kuwafikishia wengine kwa njia sahihi. Nitawafundisha ukweli, ili muweze kuufahamu. Nitawafundisha upendo, ili mjue upendo wa kweli ni kitu gani. Wanangu, Mwanangu atafanya yote ili aongee kwa njia ya maneno na matendo yenu. Nawashukuru.

Wanangu wapendwa, hata leo ninawaalika: muwe sala. Sala iwe mabawa kwa ajili ya mkutano kati yenu na Mungu. Ulimwengu upo katika wakati wa kujaribiwa, kwa maana umemsahau na kumwacha Mungu. Kwa hiyo wanangu, muwe wale wanaomtafuta na kupenda Mungu kuliko yote. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwaongoza kwa Mwanangu, lakini ninyi hamna budi kunena "NDIYO" yenu katika uhuru wa wana wa Mungu. Nawaombeeni na kuwapenda, wanangu, kwa upendo usio na mwisho. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.

To compare Medjugorje messages with another language versions choose

 

PC version: This page | Medjugorje | Apparitions[EN]  | Our Lady of Medjugorje Messages  | Medjugorje News & Articles[EN]  | Pictures & Photos[EN]  | Medjugorje Videos[EN]